KILIMO BORA CHA NYANYA
Nyanya ni aina ya mboga inayo
zalishwa kwa wingi sana duniani. Kwa Tanzania, nyanya ni zao la kwanza
katika mazao ya mboga linalo limwa na kuliwa kwa wingi ukilinganisha na
mboga zingine. Nyanya hutumika karibu Katika kila mlo. Kulingana na
umuhimu wa zao hili kama chakula na pia kama zao linalomwingizia kipato
Mkulima, kuna haja ya kutoa mafunzo kuhusu mbinu bora za uzalishaji
wake. Pia kuna umuhimu wa kufundisha wakulima kutoka sehemu zingine
wasiolima zao hili ili nao waweze kuzalisha nyanya na hivyo kuongeza
idadi ya aina za mboga katika maeneo yao.
MAHITAJI YA ZAO LA NYANYA
Nyanya hustawi vizuri kwenye maeneo ya joto, yasiyo na ukungu mwingi
hasa wakati zao linatoa maua na matunda. Zao hili hupenda kipindi kirefu
cha jua na joto ili kuongeza ukuaji wa matunda na kupunguza magonjwa ya
aina ya ukungu/kuvu. Zao hili halipendi mvua nyingi ingawa linahitaji
maji kwa wingi. Katika kipindi chenye mvua nyingi na jua kidogo nyanya
hushindwa kutoa maua na matunda ya kutosha bali huweka majani mengi.
Katika kipindi hiki pia, nyanya hushambuliwa sana na magonjwa ya ukungu.
Nyanya hupendelea udongo unaopitisha maji kwa urahisi na wenye rutuba
ya kutosha na hivyo hupenda samadi. Udongo uwe umetifuliwa vya kutosha
kuruhusu mizizi kushika vema.
AINA ZA NYANYA
Kuna aina kuu
mbili za nyanya kulingana na ukuaji wa mmea: yaani nyanya inayo refuka
zenye kuhitaji egemezi (mfano Money maker) na aina ya pili ni nyanya
fupi zenye kutoa matawi mengi mfano Roma na Cal J.
UKUAJI WA MICHE
Miche ya nyanya huzalishwa kwenye kitalu kwa kupanda mbegu. Mbegu za
nyanya huota baada ya siku 5 hadi 10. Baada ya kukua kitaluni kwa muda
wa wiki 4 hadi 5 toka kuota kwa mbegu, miche hupandwa shambani. Kabla ya
kupandikiza shambani miche huandaliwa kwa kupunguza umwagiliaji maji
kwa siku moja au mbili ili miche izoee hali ngumu kabla ya kuhamishiwa
shambani. Hapo shambani miche hupandikizwa kwa kuzamishwa katika kina
kirefu zaidi ya ilivyo kuwa kitaluni. Hii inasaidia miche kutoa mizizi
ya pembeni mingi zaidi kwa ajili ya kufyonza maji pamoja na virutubisho
aridhini. Baada ya kupandikiza mwagilia maji ya kutosha. Usimwagilie
maji juu ya mche wa nyanya. Katika kipindi cha jua kali, tandaza nyasi
kwenye tuta ili kupunguza upotevu wa maji na unaweza kuweka kivuli kwa
kutumia majani ya miti au migomba. Kulingana na aina ya nyanya na rutuba
ya udongo, nafasi ya kupandia ni sm 60 kati ya mstari hadi mstari na 45
hadi 60 nafasi ya mche hadi mche. Kama udongo hauna rutuba ya kutosha
inapendekezwa kutumia nafasi kubwa ya kupanda.
UTUNZAJI
Nyanya
fupi zisizo refuka kwenda juu, ni rahisi sana kutunza na hazihitaji
huduma nyingi. Tatizo kubwa ni kuwa kwa kutambaa chini, katika kipindi
cha mvua huwa karibu na magonjwa yatokanayo na udongo. Katika kipindi
cha jua kali, matunda huungua kwani mmea huwa na majani machache tu
yanayo kinga matunda yasipigwe na mionzi ya jua.
MBOLEA
Licha ya
mbolea ya kupandia, unashauriwa kuongeza mbolea kipindi cha wiki mbili
au tatu baada ya kupandikiza miche bustanini. Mbolea hii ya kukuzia
iwekwe kuzunguka shina la mmea kwa umbali wa sentimeta 5 hadi saba
kutoka kwenye shina. Kwa mbolea kama vile CAN, NPK, au SA tumia kifuniko
kimoja cha soda kwa shina. Mbolea hii inaweza kuwekwa mara mbili kabla
ya mvuno wa kwanza. Ili kurefusha kupindi cha uzaaji wa zao la nyanya
(na hata mazao mengine yatoayo matunda kama vile nyanya chungu,
biringanya, pilipili hoho, nk) inapaswa kuongezea mbolea katika kipindi
cha uvunaji mfano baada ya kuvuna mara mbili unashauriwa kuongeza mbolea
ya samadi na mbolea kama vile NPK. Hii inasaidia mmea kuendelea kutoa
maua bila kuchoka. Kwa kawaida nyanya fupi jamii ya “Roma” huweza kuzaa
na kuvunwa kwa kipindi cha wiki 6 hadi 8 tu. Lakini kama utakuwa
unaongezea mbolea na kukazania matunzo ya bustani (hasa usafi wa bustani
na Kumwagilia maji ya kutosha), nyanya zinaweza kuendelea kuzaa kwa
muda mrefu zaidi. Hii ni tofauti
na mazoea ya wakulima wengi kuwa
mara nyanya zianzapo kuzaa huduma za palizi na usafi wa shamba huachwa
na kutilia maanani kazi ya kuvuna pekee. Hii inajitokeza zaidi kwenye
aina ya nyanya fupi.
Kwa nyanya fupi ni vizuri kuhakikisha kuna
matawi mengi iwezekanavyo ili kuweza kupata matunda mengi zaidi. Hivyo
usipunguze matawi katika aina hii ya nyanya. Kwa nyanya ndefu zenye
kuhitaji egemezi,tunashauriwa kukuza nyanya kwa tawi moja lisilo na
vichipukizi pembeni au matawi mawili na kuacha mnyanya urefuke.
Kupunguza majani ni muhimu pia katika kupunguza maambukizo ya ukungu katika shina na pia kutoa nafasi ili
mwanga kupenya na kuruhusu mzunguko wa hewa. Majani yapunguzwe kipindi
cha asubuhi kwa kutumia mkono na siyo kisu kwani kinaweza kueneza
magonjwa kutoka mche hadi mche. Kwa nyanya ndefu, majani ya chini ya
matunda huondolewa kadiri unavyo endelea kuvuna. Unashauriwa upunguze
majani wakati wa asubuhi kwa kutumia mkono na pia usitoe zaidi ya majani
matatu katika mmea kwa mara moja.
UMWAGILIAJI
Nyanya ni zao
linalohitaji maji mengi sana kwa ajili ya ukuaji wa mmea na matunda
yake. Umwagiliaji uwe wa kulingana kwa kila siku iliyo pangwa.
Usibadilishe ovyo kiasi cha maji na ratiba ya kumwagilia. Hii
inasababisha kuoza kwa kitako cha nyanya. Pia ili kutunza maji katika
udongo, inashauriwa kuweka matandazo katika mzunguko wa shina la nyanya
au bustani yote. Nyanya inayo kua vizuri hutumia maji lita mbili kwa
siku
katika kipindi cha jua kali. Hivyo katika umwagiliaji ni busara
kuzingatia kiasi hiki cha maji katika kipindi kama hiki. Pia kama
unatumia keni, mpira au bomba usimwagilie maji juu ya matawi ya nyanya
kwani umwagiliaji wa namna hii utasababisha kuenea kwa magonjwa ya
ukungu.
MATATIZO YA KILIMO CHA NYANYA
Matatizo yanayosumbua
kilimo cha zao hili ni magonjwa na wadudu waharibifu. Hapa tutajifunza
mbinu mbali mbali za kuzuia magonjwa na wadudu waharibifu.
WADUDU WAHARIBIFU
FUNZA WA NYANYA (Funza wa vitumba)
Huyu funza hushambulia mazao mengine kama vile pamba, mahindi, mtama,
maharage n.k. Mdudu huyu hushambulia matunda ya nyanya kwa kutoboa na
hivyo kuyafanya yapoteze soko kwasababu hayafai kuuzwa katika soko na
pia yanaweza kuoza wakati wa usafirishaji. Ili kuthibiti piga dawa ya
kuua wadudu kama vile thiodan, sevin ya unga, karate, selecron, n.k.
Muarobaini hutumika pia katika kupunguza uharibifu wa mdudu huyu.
INZI WEUPE
Wadudu hawa huruka ruka kwenye shamba la nyanya na kukaa chini ya
majani. Mdudu huyu hueneza magonjwa ya virusi kama vile “ukoma wa
nyanya”. Usafi wa shamba na mazingira ya yake ni muhimu katika kupunguza
kuzaana kwa wadudu hawa. • Ili kuthibiti wadudu hawa kwenye bustani ya
mboga na pia katika maficho yao, piga dawa kama vile karate,
cypermethrin mara kwa mara. • Panda mimea mingine (kama vile tumbaku)
inayo vutia wadudu hawa kwenye maeneo ya bustani kisha piga dawa katika
miche ya tumbaku ili kuwaangamiza kwa wingi.
MINYOO
Mdudu huyu
hukaa kwenye udongo wenye unyevu wa kutosha. Huvamia mizizi ya nyanya na
kuharibu mfumo wa usafirishaji maji na chakula kwenye nyanya iliyo
athirika. Uking'oa mche wa nyanya utaona vifundo kwenye mizizi.
KUZUIA
Mbinu za kuthibiti ongezeko la wadudu hawa ni kuharibu hali ya udongo
inayo mfanya aishi na kuzaana. Mbinu hizi ni: • Kulima shamba kwa
kutifua baada ya kuvuna nyanya ili udongo wa chini ukae juani na
kukauka. Hii inasaidia kuangamiza wadudu hawa kwa joto na ukosefu wa
maji. • Choma moto na kuteketeza mabaki ya nyanya baada ya kuvuna. •
kuzungusha aina ya zao la nyanya au jamii ya nyanya na mazao mengine
yasiyo vamiwa na adui huyu. Hii huwafanya minyoo wasipate hifadhi na
chakula kutoka kwenye mimea wanayo tumia kuishi na kuzaliana. Hivyo
idadi yao kupungua katika udongo. • kabla ya kupanda zao weka samadi
nyingi katika udongo kwenye eneo lililo athiriwa na wadudu hawa kwani
hawapendi udongo wenye samadi nyingi. • Panda manung'a nung'a (Tagetes
spp) katika eneo lililoathirika na minyoo hawa, mimea hii hutoa sumu ya
aina fulani ambayo huathiri ukuaji na kuzaliana kwa minyoo hawa.
MAGONJWA
Uchunguzi umeonyesha kuwa katika maeneo ya Kilombero na Gairo, nyanya
na mazao mengine jamii ya nyanya ndiyo hushambuliwa sana na magonjwa
kuliko mazao mengine ya mboga.
UKUNGU
Huu ni ugonjwa unaopenda
hali ya unyevu mwingi hewani. Hivyo hujitokeza zaidi wakati wa masika.
Pia sehemu zenye umande mwingi wakati wa usiku, ugonjwa huu hujitokeza
hata wakati wa kiangazi.
DALILI ZAKE
Ugonjwa huu hushambulia
shina, maua na matunda. Kuungua kwa majani kama vile yamechomwa na maji
moto. Chini ya jani utaona unga unga mweupe. Matunda pia hushambuliwa na
ugonjwa huu na hugeuka kuwa meusi na magumu.
KUZUIA
• Inabidi
kuchanganya mbinu mbali mbali za kupambana na ugonjwa huu. • Kwanza ni
usafi wa shamba kwa jumla yaani hakikisha unaondoa magugu katika
bustani. • Tandaza nyasi juu ya matuta yaliyo pandwa nyanya. • Ondoa
majani yaliyo zeeka na yanayo onyesha dalili za ugonjwa huu. katika
kupunguza majani, hakikisha sehemu za chini ya mmea ni wazi na kuna
mzunguko mzuri wa hewa. Punguza majani katika mmea ili kupunguza umande
na ukungu kwenye mmea. • Baada ya kupunguza majani na machipukizi
hakikisha unatupa mbali majani hayo na siyo kuyaacha kwenye tuta la
bustani. • Ondoa kabisa mmea ulio na dalili za ugonjwa huu • Kupiga dawa
katika kipindi cha mvua mara baada ya mvua kubwa. Fanya hivyo mara moja
au mara mbili kwa wiki kutegemea na wingi au mfululizo wa mvua.
Unapoona jua limetoka piga dawa ili ugonjwa usijitokeze tena. Baadhi ya
madawa yanayofaa kukinga ugonjwa huu ni Dithane M45, Bravo, Benlate ,
Ridomil, Topsin n.k. Kumbuka kuwa kila
mwaka madawa yenye nguvu
zaidi hutengenezwa, hivyo uliza watalaam walioko karibu nawe. Ingawa
Blue Copper inauzwa kwa bei nafuu, nguvu yake in kidogo sana kuthibiti
huu ugonjwa. Muarobaini pia unaweza kutumika kupunguza ugonjwa huu.
Changanya unga unaotokana na mbegu za muarobaini kiasi cha nusu kilo ya
unga katika lita 20 za maji.
UKOMA WA NYANYA
Huu ni ugonjwa wa
virus unao enezwa na inzi mweupe. Inzi hawa hushambulia zaidi nyanya
wakati wa kiangazi, hasa kipindi cha joto kali.
DALILI
• Majani
machanga hujikunja na baadaye majani yote. • Kupungua kwa utoaji maua na
matunda na hata yakitokea matunda huwa ni madogo. • Mmea kudumaa na
kutozaa kabisa.
KUZUIA
Mbinu madhubuti ni kupunguza
kuenea kwa ugonjwa huu kwenye shamba kwa kudhibiti kuzaana na kuenea kwa
mdudu (inzi mweupe) kama tulivyo ona katika kupambana na mdudu huyo,
yaani: • Kuondoa mimea michache iliyo shikwa na ugonjwa maana wadudu
hawa wanachukua ugonjwa huu kutoka mimea hii. • Kutumia mbegu zilizo
hakikishwa kuwa zinaweza kuvumilia ugonjwa huu na kutoa mavuno mazuri. •
Usilime nyanya karibu na eneo lililo na mazao kama bamia,mipapai maana
mimea hii huhifadhi inzi mweupe. Kuua inzi weupe wanaofyonza nyanya na
kusambaza virusi kwa kutumia madawa. Tumia madawa kama vile Selecron,
Decis, Karate n.k. • Epuka kuchanganya zao la nyanya na mazao mengine
yanayohifadhi hawa nzi kama vile mipapai na bamia. • Ng'oa na kuchoma
moto mimea yote iliyougua ugonjwa huu.
UGONJWA WA KUOZA SEHEMU YA SHINA INAYOGUSA UDONGO NA MMEMA KUNYAUKA KAMA UMEKOSA MAJI
• Wadudu wanaosabisha ugonjwa huu hupatikana ardhini. • Hakuna dawa ya kutibu ugonjwa huu baada ya dalili
kujitokeza. • Kupiga madawa za viwandani ardhini kabla ya kupanda
nyanya husaidia kupungu wadudu wa ugonjwa. • Epuka kupanda nyanya au
mazao jamii ya nyanya katika eneo moja kwa muda mrefu mfulilizo. Baadhi
ya mazao yanayohusiana na nyanya ni bilinganya, pilipili, ngogwe, mnavu,
n.k.
Ugonjwa wa miche michanga ya nyanya kuoza sehemu ya shina inayogusa udongo na kufa ghafla
Ugonjwa huu hushambulia miche kitaluni na husabishwa na wadudu waishio
ardhini. Mara baada ya dalili, ugonjwa huu hauna dawa ila unaweza
kukingwa kwa kutumia njia zifuatazo: • Choma moto udongo wa kutengenezea
kitalu kabla ya kupanda mbegu zako. Kutumia mboji husaidia kukinga
miche dhidi ya ugonjwa huu. • Epuka kumwagilia maji kupita kiasi na
kutumia kuvuli kizito
MATUNDA YA NYANYA KUOZA KITAKO
Huu ni
ugonjwa unaosababishwa na: • Umwagiliaji wa nyanya bustanini usio na
mpangilio maalumu. Mfano, kumwagilia mimea maji mengi kisha kuiacha bila
maji kwa siku kadhaa. • Upungufu wa virutubisho aina ya chokaa. Dalili
zake ni matunda ya nyanya kuoza sehemu ya kitako na kuonyesha rangi
nyeusi. Kuzuia ugonjwa huu, zingatia kuwa na utaratibu mzuri wa
kumwagilia maji ambao haubadiliki ovyo kiratiba na kiasi cha maji
yanayowekwa. Rutubisha mimea kwa madini ya chokaa kwa kutumia mbolea aina ya CAN zenye madini haya.
0 Response to " "
Post a Comment